Tanzania-Waziri Hasunga akutana na AGRI-CONNECT
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga amekutana na wajumbe kutoka Umoja wa Jumuiya ya Nchi za Ulaya hapa nchini wakiwa wameongozana na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.
Lengo ni kupitia na kukubaliana maeneo ya Utekelezaji wa Mradi kwenye Sekta ya Kilimo unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Jumuiya ya nchi hizo (European Union Development Fund ) kupitia progamu ya “AGRI Connect supporting value chains for shared prosperity.”
Wakiongea katika mkutano huo uliofanyika katika Ofisi ya Waziri,walimueleza Mhe. Hasunga kwamba mradi huo wa Agri Connect utakuwa ukitekelezwa kwa muda wa miaka minne kuanzia 2020-2023 ambapo utagharimu EURO Millioni mia moja.
Aidha Mradi wa Agri Connect utashughulikia mazao matatu ambayo ni Kahawa, Chai, na mbogamboga (horticulture) na vikolezo.
Huko, Zanzibar watashughulikia suala la kuongeza mnyororo wa thamani, (value chain) kuwajengea uwezo wadau na wakulima na kuboresha masuala ya lishe.
Maeneo ya mradi huo ni Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe na Katavi wakati kwa upande wa Zanzibar ni Unguja na Pemba. Wakitoa taarifa yao kwa Waziri wa kilimo timu hiyo imesema kwamba mradi wa Agri Connect utatekelezwa na makampuni matano ambayo yalishinda zabuni ambapo yatawajengea uwezo wakulima zaidi ya 10,000 wa maeneo ya mradi.
Wamebainisha kwamba mradi huo utagharimu kiasi cha EURO 52 millioni na kiasi cha EURO 48 Milioni zitatumiwa na wakala wa barabara TARURA kwa ajili ya kujenga miundombinu ya barabara katika maeneo ya mradi ili kufanikisha mnyororo wa kuongeza thamani kwa mazao hayo.
Mhe Waziri aliwashukuru na kuwaeleza kwamba mradi huo ulenge Zaidi kwenye kuhamisha na kuimarisha tecknolojia za uzalishaji na masoko ya bidhaa za wakulima kwa kila zao ambapo kampuni moja kati hayo lishughulikie mazao ya mbogamboga ,viungo na vikolezo .